Trevor Tony

Saturday, May 14, 2022

Historia ya vita Kati Ya Majeshi Ya Uingereza dhidi ya majeshi ya kijerumani katikati ya nchi ya Tanganyika eneo la mto Rufiji

Tarehe 4 Januari 1917, vita ilikuwa imepamba moto. Majeshi wa Uingereza dhidi ya majeshi ya kijerumani katikati ya nchi ya Tanganyika eneo la mto Rufiji.



Askari wa kingereza, jina lake Frederick, alikuwa amejificha mahali kukabiliana na askari wa kijerumani. Akachukua "darubini" kutazama ni wapi walipo maadui. Ile anainua shingo tu, anakula risasi moja ya kichwa na kufariki papo hapo.

-------------------------

Baada ya kusikia taarifa za kuuwawa kwa Fredrick, Rais wa Marekani, bwana "Theodore Roosevelt", alihuzunika sana maana alikuwa ni rafiki yake kipenzi. Roosevelt aliandika ujumbe mzito kuonesha masikitiko ya kumpoteza rafikiye. Mwili wa askari huyo ulizikwa hapo hapo na kaburi lake lipo hadi leo hii.

Frederick, mbali na kuwa askari katika jeshi la Uingereza, alikuwa mwindaji. Alizaliwa Uingereza na kuja Afrika kwa Shughuli za upelelezi "exploration". Lakini pia kwa shughuli za uwindaji. Alikuwa mwindaji maarufu sana ulimwenguni, akianzia maeneo ya Afrika Kusini, Zimbabwe hadi Tanganyika.

"Aliua sana wanyama wetu".

Akiwa Tanganyika enzi hizo koloni la Ujerumani, Fredrick alipambana dhidi ya askari wa kijerumani katika maeneo mbalimbali ikiwemo maeneo ya kuzunguka mto Rufiji ambapo ndipo kuna pori alilokuwa akiwinda wanyama. Pori hilo lilianzishwa mwaka 1896 na serikali ya Ujerumani chini ya gavana Von Weissman. Mwaka 1905, pori hilo lilifanywa kuwa maalumu kwa shughuli za uwindaji.

Baada ya vita, Uingereza ilishinda na kutwaa koloni la Tanganyika. Na ili kumuenzi kapteni Fredrick Selous, mwaka 1922, serikali ya kikoloni ya Uingereza iliamua kugeuza pori hilo kuwa pori la hifadhi la Selous kwa kingereza "Selous Game Reserve".

Kaburi lake limo ndani ya pori hilo katika eneo la Beho-beho.

Hivyo, tumejua kwamba "hifadhi ya wanyama pori ya Selous (seluu)" imepata jina hilo kutokana na huyo Fredrick Selous.

Ahsante.
 According  to KichwaKikuu

HISTORIA ITAHIFADHI MCHANGO WETU KATIKA KUJENGA JAMII MPYA YENYE KUFIKIRI.

Hayo ni maneno ya raisi wa kwanza wa nchi ya Msumbiji, Hayati Samora Machel ambaye alifariki katika ajali ya ndege ‘Yenye Utata’ tarehe kama ya Leo 19 octoba, 1986 yaani miaka 32. Wakati wa uhai wake, aliweza kubadili mbinu za kuondoa ukoloni kutoka vita vya msituni mpaka mapinduzi yaliyong’oa utawala wa kireno.

Aliamini katika dhana ya ujenzi wa jamii mpya yenye namna yake ya kufikiri; Mara kadhaa katika hotuba zake alirudia kuwa jamii yoyote haiwezi kwenda mbele kama haiwezi kubadilika kwa mfumo wa kufikiri wa watu wake.

Samora Machel ni nani?

Machel alizaliwa mwaka 1933 na kukulia katika kijiji cha Chilembene, wazazi wake walikuwa masikini sana na walikuwa wa kabila maarufu la Shangana ambalo lilipigana vita vikali dhidi ya wareno kwenye karne ya 19. Akiwa na miaka 17 tu familia yake ilipokonywa eneo walilokuwa wakiishi na kulima, shamba hilo alipewa Mlowezi wa kireno. Hivyo ndugu zake akiwemo kaka yake mkubwa alikimbilia kwenye migodi ya madini nchini Afrika ya Kusini ili kuweza kumsaidia Samora Machel aweze kuendelea na masomo. 

Kwa bahati mbaya, Kaka yake huyo alifariki mgodini kwenye ajali iliyouwa vibarua kadhaa kati ya miaka ya 1950.
Samora Machel alisoma fani ya Unesi, alihudhuria vipindi mpaka mchana. Na jioni alikwenda kufanya kazi katika mashamba ya pamba kama kibarua ili kuweza kukabiliana na hali ngumu ya maisha. Fani ya unesi na ualimu zilikuwa na nafasi chache tu za kazi kwa waafrika. Alivutiwa taratibu na mawazo ya kijamaa, alipoajiriwa alianza kuongoza migomo kupinga manesi weusi kulipwa mshahara mdogo kulinganisha na Manesi wa kireno.
Mara kadhaa alihoji ‘Ni kwanini mbwa wa Mreno anapata huduma bora za chanjo na madawa kuliko wafanyakazi ambao huumia kuhakikisha Mreno anapata utajiri zaidi’. Hkukuwa na majibu toka kwa wanyonyaji. Alikata shauri akiwa na miaka 29, aliacha kazi na kujiunga na FRELIMO ili kupigania uhuru wa Msumbiji, alikimbilia Botswana kisha kufika Tanzania kupata mafunzo maalumu ya kijeshi.

Mwaka 1963, alikuwa mmoja ya watu waliopelekwa Algeria kupata mafunzo ya juu ya kijeshi(Alitumia pasipoti ya Tanzania). Aliporudi alipelekwa eneo la kongwa(Dodoma) kwenye kituo cha mafunzo cha FRELIMO huko alikuwa mkufunzi.

Mwaka 1964, alienda kaskazini mwa Msumbiji kuongoza vita vya msituni dhidi ya Wareno, Baada ya kifo cha Filipe Magaia, Machel alichaguliwa kuwa mkuu wa majeshi ya FRELIMO mwaka 1966. Miaka mitatu baadae(1969) Edwardo Mondlane aliyekuwa raisi wa FRELIMO aliuliwa mjini Dar es Salaam kwa bomu lililofichwa kwenye bahasha. Hali ilikuwa ni ya kutisha kwani serikali ya Kikoloni ya Msumbiji ilikuwa ‘ikiwawinda’ viongozi wa FRELIMO lakini hilo halikumtisha Samora Machel, aliteuliwa kuwa mkuu mpya wa FRELIMO na kuchukua majukumu hayo kwa ujasiri. 

Jeshi la serikali ya Msumbiji lililokuwa chini ya Wareno lilifanya uhasi mwaka 1974, tukio hilo lilidhoofisha serikali hiyo. Machel aliongoza mapambano na hatimaye tarehe 25 Juni, 1975 Msumbiji ikawa nchi huru. Katika hotuba yake alisema, "Kati ya mambo mengi tuliyofanya historia itatukumbuka kwa mchango wetu kama kizazi kilichobadili mbinu za mapambano dhidi ya adui, yaani mapinduzi kisha tukajua jinsi ya kujenga fikra mpya(Namna ya kufikiri) kisha tukajenga jamii mpya iliyo huru!

Kwa haraka alitaifisha mashamba na mali zote za Wareno zilizokuwepo Msumbiji, Kukawa na zama mpya kabisa. Aliongoza kujengwa kwa hospitali, shule na vyuo vya ufundi ili kuimarisha sekta zote za nchi yake! Ghafla kundi la RENAMO liliendesha hujuma dhidi ya miundo mbinu mipya iliyojengwa na serikali ya FRELIMO, Machel hakuwa tayari kuendesha vita vya ndani dhidi ya RENAMO. Alijaribu njia ya mazungumzo na kutokana na juhudi zake alitunukiwa tuzo ya amani ya Lenin(Lenin Peace Prize 1975-1976).

Pamoja na changamoto zote, Samora Machel alishirikiana na wapiganaji wa ukombozi wa Nchi za Afrika ya kusini na zimbabwe(Ilikuwa inaitwa Rhodesia Kusini). Hili liliwakera mno wazungu wakoloni hasa makaburu wa Afrika kusini. Mara kwa mara kulitokea mapambano kwenye mipaka.

Iliaminika kwamba, Samora Machel alikuwa ni tishio kubwa kwa makaburu! Mbinu zake na misaada aliyotoa kwa wapigania uhuru zilikuwa na athari kubwa. Serikali ya kikaburu mara kadhaa alilaani hujuma ilizofanyiwa, mara zote ilihusisha serikali ya Msumbiji na marafiki wake wakubwa Tanzania(Pia Wapiganaji wa ANC walikuwepo Mazimbu, Tanzania na maeneo mengine.

Tarehe 6, Mwezi Octoba,1986 kulitokea mlipuko uliojeruhi askari sita wa jeshi la Afrika kusini(SADF). Haraka waziri wa Ulinzi wa serikali ya kikaburu, Jenerali Magnus Malan alihusisha serikali ya Msumbiji, alidai
‘Kama raisi Machel ameamua kutumia vilipuzi vya ardhini nasi tutajibu mapigo ipasavyo, Hatutavumilia hili’
Aliongea hayo kwa lugha ya Afrikana, na kutafsiriwa kwa kiingereza. Mamlaka za usalama za ndani hazikuchukulia kwa uzito madai hayo.

Kulingana na nyaraka za idara ya habari ya ndani(Nina documents chache) inaeleza kuwa Mlipuko uliotokea Kingwane bantu na kujeruhi askari wa Afrika ya Kusini haukupangwa wala kujulikana na Samora Macheli.

Wiki mbili baadaye yaani tarehe 19 Octoba 1986, alipokuwa akitokea kwenye mkutano nchini Zambia alipata ajali karibu kabisa na eneo palipotokea mlipuko wa Kingwane bantu.
Ndege ya raisi Machel aina ya Tupolev Tu-134 ilianguka kwenye milima ya Lebombo ndani ya eneo la Mbuzini ambalo ni la Afrika Kusini. Kulikuwa na majeruhi tisa, Lakini raisi Samora Machel na maofisa wengine 24 walifariki dunia.

Kifo chake kilishtua Ulimwengu, Serikali ya kikaburu ilitangaza kuwa ile ilikuwa ni ajali ya ‘Kawaida’ . Tukio hilo lilimuumiza sana baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu Nyerere! Alionekana kulia mbele ya Uma baada ya kupata taarifa hiyo.

Huko Afrika ya Kusini, Malawi na Zimbabwe makundi ya vijana yaliingia mitaani na kufanya maandamano makubwa. Mjini Harare, Vijana walichoma na kuharibu mali zinazohusishwa na makaburu. Waliamini kwa vyovyote vile Makaburu walihusika na ajali hiyo. 
The Mozambique News Agency(AIM) ambayo imekusanya taarifa mbalimbali, ikiwemo mawasiliano ya ndani kabisa. Kwa maelezo yaliyopo ndege haikuanguka kutokana na hali ya hewa au tatizo la kiufundi kulingana na kisanduku cheusi cha ndege(BLACK BOX). Hivyo basi, inawezekana kabisa Magnus Malan ambaye alikuwa waziri wa serikali ya kikaburu alikuwa nyuma ya tukio hilo. Karibu kabisa na Mbuzini ilipoanguka ndege, kulikuwa na kituo kidogo cha jeshi la Afrika ya kusini kilichokuwa kikilinda eneo la mpaka linalounganisha nchi za Msumbiji, Botswana na Afrika Kusini.

Bado kuna maswali mengi juu ya ajali hii. Kwa leo Niishie hapa!

According To Francis Daudi


Picha Historia: Ya Mwalimu Nyerere ziarani Bangalore, nchini India

Hii ni picha ya kumbukumbu ipo katika kiwanda cha helikopta, Bangalore!

Inamwonesha Raisi wa kwanza wa Tanzania, Hayati Mwl. Nyerere na ujumbe wake walipotembelea India kwa ziara ya kiserikali na kufika hapo kiwandani tarehe 20 Januari, 1976.

Hindustan Aeronautics Limited (HAL) pia kinaitwa Chetak ni kiwanda ambacho bado kinaunda chopa au helikopta mpaka leo na kipo chini ya wizara ya ulinzi ya Taifa la India.
Ni jambo la furaha kuona wenzetu wameweka kumbukumbu hii nzuri!

Hakika Historia ni somo zuri sana na historia ni somo linaloishi. Na ndio maana Marcus Garvey aliwahi kusema," Watu wanaoishi bila kujua Historia na utamaduni wao ni sawa na mti usio na mizizi"

Francis Daudi